
Mara nyingi unaweza kukuta mtu ana
kabati limejaa nguo hadi zinakosekana pa kuwekwea na katika hali halisi
anajiona hana nguo za kuvaa. Hali hii inatokana na kukosa mpangilio wa
nguo kwenye kabati na pia kuweka nguo ambazo hazihitajiki tena. Nguo zisipokuwa
na mpangilio maalumu ni ngumu sana kutafuta nguo gani uivae na ipi maana hujui
ipo upande gani wa kabati. Pia pale unapohifadhi nguo ambazo unajua hutazivaa
tena inasababisha kabati kujaa bila sababu. Njia hizi zitakusaidia katika
kupanga kabati lako:
1. Tafuta siku ambayo unamuda wa
kutosha na toa nguo zako zote kabatini kisha tenga zile ambazo unahitaji
kuzivaa na zile ambazo unaona hutazivaa tena ( iwe zimekubana, zimechakaa,
hauzitaki tena n.k).
2. Tafuta mfuko safi uweke nguo zote
ambazo hutazivaa tena ambazo upo tayari kugawa kwa wenye uhitaji. Ni vyema
ukianzia nyumbani mwako, kama una dada wa kazi unaweza mpa zile ambazo zitamfaa
na kisha nyingine ukapelekea wengine wenye mahitaji unaowafahamu kama ni
kanisani au mahali popote pale. Ila jihadhari usimpe mtu nguo iliyochakaa sana,
haipendezi.
3. Nguo ambazo unazihitaji zitenge
katika makundi (blauzi, sketi, magauni, n.k) na kisha uzikunje vizuri na
kuzipanga kabatini kila kundi sehemu yake. Hii itakusaidia ukiwa unatafuta
gauni unajua uangalie sehemu gani. Nguo zinazoendana pamoja kama suti au
vitenge ni vyema zikawekwa pamoja sketi na blauzi yake. Kama kabati lina nafasi
kubwa makoti ya suti yakiwekwa kwenye henga yanapendeza zaidi.
4. Vitu kama mikanda, skafu, mitandio
n.k viwekwe mahali pake ili iwe rahisi kupatikana pale vinapohitajika.
Jitahidi
uwe na tabia ya kupanga nguo zako kila unapozifua. Ilikuepuka kutafuta nguo
asubuhi na hatimaye kuharibu mpangilio wa kabati lako ni vyema kama utakuwa na
utaratibu wa kunyoosha nguo za wiki zima kila mwisho wa wiki, hii itaokoa muda
na ‘stress’ za kutafuta nguo ya kuvaa kila asubuhi.
by AGUSTINO HAMIS
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni