Jumanne, 23 Mei 2017

Lwandamina atoa mustakabli wa usajili mpya msimu ujao

Lwandamina atoa mustakabli wa usajili mpya msimu ujao


George Lwandamina kocha mkuu Yanga SC amesema kikosi chake cha Yanga SC kinahitaji mabadiliko makubwa kuendana na hadhi ya klabu hiyo kitaifa na kimataifa.
Baada ya kuvunja kambi rasmi atakabidhi ripoti nzima ya ligi kwa uongozi na kwa ushirikiano watajua jinsi gani watakiboresha kikosi hicho kwa ajili ya msimu mpya wa ligi Tanzania 2017-18 utakaoanza mwezi August mwaka huu.
Yanga SC wanatarajiwa kuvunja rasmi kambi yao wiki ijayo baada ya ziara yao mikoani inayoanza rasmi kesho. Kesho wataondoka mapema jijini Dar kuelekea Dodoma na mwishoni mwa wiki watakuwa jijini Arusha .
Yanga SC wameibuka mabingwa wa ligi kuu msimu huu ikiwa ni mara ya tatu mfululizo 2014-15,2015-16 na msimu huu 2016-17.
Kipindi chote cha msimu huu wa ligi kuu Tanzania bara Yanga licha ya kuibuka mabingwa lakini bado walikuwa wakionesha udhaifu nafasi mbalimbali katika kikosi chao.
Kiungo cha chini limekuwa tatizo sugu katika kikosi hicho toka alipokuwepo bwana Hans Van Pluijm . Licha ya utitiri wa viungo katika klabu hiyo lakini bado hawajapata mtu sahihi kuiendesha vyema timu eneo hilo. Kuondolewa kwa Mbuyu Twite na kuletwa Justine Zulu toka Zesco United bado hakujatibu tatizo hilo sugu ambalo lilianza mara baada ya viungo Athuman Chuji na Frank Domayo kuondoka katika kikosi hicho.
Justine Zulu majeraha ya mara kwa mara na kukosa match finess kwa kipindi kirefu kumemfanya kucheza chini ya kiwango pia kukosekana mara kwa mara kwenye kikosi hicho. Juma Saidi ‘ Makapu ‘ aliyeanza kukuzwa vyema na Maximo katika kikosi hicho bado hajalitendea haki eneo la kiungo cha chini . Mara nyingi amekuwa akipanda na kushuka katika kiwango chake pia majeraha ya mara kwa mara.  Muunganiko wa viungo wachezeshaji Haruna Niyonzima na Thabani Kamusoko ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo , wamegeuka msaada mkubwa kuisaidia nafasi hiyo. Hivyo ni dhahiri Lwandamina anakwenda kuliangalia upya eneo hili ili awe imara na kikosi chake msimu ujao.
Beki ya kushoto ya timu hiyo imekuwa ikimtegemea zaidi Haji Mwiji na mbadala wake Oscar Joshua kuonekana umri unamtupa mkono na kasi yake kupungua . Mara nyingi Mwinyi akiwa mgonjwa au kuchoka kutokana na fatigue timu inayumba katika nafasi hiyo . Hivyo ni dhahiri Lwandamina ataliangalia pia eneo hilo.
Safu ya walinzi wa kati wanaposimama Nadir Haroub , Vincent Andrew, Kelvin Yondani na Vicent Bossou napo panahitaji jicho la kipekee . Nadir mwenye miaka 11! katika kikosi hicho anaonekana kuanza kuchoka sanjari na pacha wake Kelvin Yondani ambaye nae umri umesogea ingawa bado uwezo upo . Lwandamina anahitaji damu changa yenye kasi na uchu wa mafanikio kwa ajili mustakabali mpya wa klabu hiyo kwa miaka mitatu au mitano ijayo.
Wing ya kulia ya timu hiyo amebaki Saimoni Msuva tu katika ubora wake na mara kwa mara tumeona akiumia timu inapwaya na kukosa mtu wa kaliba yake. Juma Mahadhi aliyesajiliwa msimu huu amekosa mwendelezo mzuri wa kipaji chake katika timu hiyo. Ana uwezo wa kucheza kama winga wa kulia na kiungo mshambuliaji lakini mara kwa mara kapewa nafasi na kushindwa kuonesha upinzani halisi kwa Saimoni Msuva au Haruna Niyonzima eneo la kati . Bado kijana mdogo ambaye akitumia vyema mapumziko haya kujijenga atafanikiwa lakini haraka ya mafaniko ya Yanga SC katika ligi inazoshiriki ni mtihani kwake . Lwandamina anahitajika pia kuangalia mbadala sahihi wa Saimoni Msuva ili kuleta ushindani halisi wa namba kikosini na kuiweka vyema timu katika uwiano mzuri wa wachezaji kikosini.
Safu ya ushambuliaji Lwandamina ana changamoto kubwa . Anapoikosa kombinesheni ya Donald Ngoma na Amisi Tambwe kikosi kinapwaya . Kama sio kupanda kwa kiwango cha Obrey Chirwa duru hili la pili la ligi kuu , Yanga ilikuwa katika hali mbaya katika eneo hilo. Kuumia kwa Donald Ngoma na Amisi Tambwe lilikuwa pigo kwa benchi la ufundi la timu hiyo na hii ilitokana kwa wachezaji kama Malimi Busungu kuikacha kambi na kuendekeza starehe na Mateo Antony kutokuwa katika ubora mzuri kuibeba timu. Upangwaji wa Obrey Chirwa kama mshambuliaji wa kati akizungukwa na viungo washambuliaji kama playmakers kwake ilisaidia kwa kiasi kikubwa .
Ni dhahiri katika ripoti yake George Lwandamina atalitazama vyema eneo hilo ili kuipa kasi timu katika ufungaji . Ni muda wa kujiuliza kuna haja ya kuendelea na baadhi ya wachezaji katika eneo hilo ? Au kuleta wapya wenye kasi na njaa ya mafaniko sio kama kina Malimi Busungu.
Lwandamina anahitajika kutulia na kukisuka kikosi vyema endapo atapata fungu zuri la usajili kipindi hiki cha mapumziko hususani kwa kuijenga timu hiyo kwa kutizama viwango vya timu ambazo atakutana nazo katika michuano ya klabu bingwa Afrika na sio ligi ya ndani.
Yanga SC imejikuta msimu huu ikiondolewa raundi ya pili katika michuano ya klabu bingwa Afrika na sababu kubwa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye viwango vya wastani kupambana kimataifa. Ni dhahiri kama wangekuwa na viwango bora wasingeondolewa na Zanaco FC kwa faida ya goli la ugenini .
Viwango vya wachezaji wa  Yanga SC na upambanaji kitimu kwa ujumla vilionekana vipo chini katika play off na MC Alger nchini Algeria . Usajili na ujenzi wa kikosi cha Yanga SC ulenge kushinda upinzani kama ule sio kuchukua alama tatu mbele ya Majimaji FC . Lwandamina huu ni wakati wake kuijenga Yanga mpya maana kikosi alichokikuta kwa asilimia 98 kilijengwa na Hans Van Pluijm
.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni